Jumapili ya 16 ya Mwaka A

So mo la Kwanza:     Hek. 12:13, 16 - 19
Wimbo Wa Katikati:    Zab. 86:5-6, 9-10, 15-16
Somo La Pili:         Rum. 8: 26 – 27
Injili:             Mt.  13: 24 – 43

Muhtasari wa Masomo:

Katika somo la kwanza, tunasikia kuwa Mungu ana uweza na uelewa wa vitu vyote na hili ndilo chimbuko la haki inayomfanya aamue kwa huruma. Matendo haya ya Mungu ni fundisho linalowalazimisha wale walio wa haki kuwa na huruma ili kuwapa watoto wa Mungu msingi wa kuwa na matumaini yatakayo washawishi kutubu dhambi zao. Katika somo la pili, Mtume Paulo anawaambia Warumi kuwa Roho huja kutusaidia katika udhaifu wetu kwani hatujui jinsi ya kusali tunavyotakiwa. Mungu anaijuia shabaha ya mioyo yetu katika Roho anayetuhimiza kuyafanya mapenzi ya Mungu. Na katika Injili, Yesu anafananisha ufalme wa Mungu na mbegu ndogo za ngano na haradhali. Pia anaufananisha Ufalme wa Mungu na amira. Yesu anatumia mifano ya mbegu na amira. Vitu vyote hivi ni vidogo sana, mbegu hizi zikirushwa ardhini huwa kama zimepotelea huko, na pia ukichanganya amira kwenye unga wa ngano, huonekana kama imepotelea huko lakini, mbegu zinapoota, huwa kubwa sana kama unga unavyoumuka ukichanganywa amira.

Tafakari:

Mbegu ya Ngano:

Mbegu ya ngano ni mbegu ndogo. Mkulima hurusha mbegu hii shambani ikishachanganyika na mchanga siyo rahisi tena kuiona. Ni kama hupotelea mchangani (ardhini). Ikisha changanyika na mchanga huwezi tena kutofautisha ni wapi kuna mbegu ni wapi hakuna. Na inapochipua, huwezi pia kutofautisha kati ya ngano na gugu. Lakini ukisubiri zaidi, tofauti huanza kujitokeza. Waswahili walisema, "Mtoto wa nyoka ni nyoka." Gugu litakomaa kama gugu na ngano kama ngano. Gugu haliwezi kuzaa ngano wala ng'ano haizai gugu. Huu ni wakati tuonaoweza kusema kuwa, mtu hujulikana kwa matunda yake. Na amira hivyo hivyo, huwezi tofautisha unga ulio na amira na usio na amira. Ni lazima kusubiri, ili unga uumuke. Maumbile yanatufundisha tuwe na subira, kuna vitu ambavyo ni lazima tusubiri hakuna njia ya mkato. Na ufalme wa Mungu ni hivyo hivyo.

Subira yavuta kheri:

Ni kitu gani basi ambacho mbegu ndogo ya haladari, ya ngano na amira vinaweza kutufundisha kuhusiana na uwepo wa Mungu duniani? Ufalme wa Mungu unashuhudiwa katika vitu vidongo vidogo na vya kawaida kabisa maishani. Kwa matendo madogo madongo yaliyotokana na muitiko wa Neno la Mungu ufalme wa Mungu hudhihirishwa. Imani na mazoea ya kufanya vitu vidogo vidogo vinavyodhihirisha imani, ufalme wa Mungu hudhihirishwa.

Ninaandika tafakari hii nikiwa ghorofa ya tatu katikati ya jiji la San Francisco, Marekani. Nikitaza dirishani ninaona Kanisa kubwa la Mt. Dominiki ambalo shrine (madhabahu??) ya Mtakatifu Yuda Thadeus ni Maarufu sana duniani. Watu hutoka Japan, China na sehemu mbalimbali duniani kuhiji na kuwa na mafungo hapa. Kanisa ni kubwa na limejengwa kwa gharama kubwa. Ni jinsi gani mambo haya makubwa yalianza? Imani, watu wa imani walijitolea kwa hali na mali, kidogo kidogo walijenga kanisa ama hekalu ukitaka kuliita hivyo ambalo ni kubwa. Mbegu ya imani yao, imeota na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani wanakuja kuhiji, kutafuta burudisho na kurutubisha imani yao. Maisha ndivyo yalivyo, tunakua kila dakika katika maisha yetu, ninapokea salamu nyingi pia siku ya leo, marafiki, wakristo wangu wa Kenya na nyumbani Tanzania wananitakia hongera ninapoadhimisha siku ya kuzaliwa na miaka sita ya upadrisho wangu siku ya leo. Kila mkristo anawajibu wa kuangalia ile mbegu ilipandwa moyoni mwake, isije ikaangamizwa na magugu. Usikate tamaa kwa kutokuiona mbegu, ama kwa kutoweza kuitofautisha na magugu. Roho wa Mungu tuliopewa anatusaidia kuomba. Atakuongoza na utawagusa wengi zaidi ya unavyofikiria.

Masomo ya leo ni ya kutupa moyo wakristo hasa tunaposhindwa kuona dalili zozote za mabadiliko katika maisha yetu ya ufuasi wa Kristo ama katika maisha ya watu. Yesu anatuambia, tusibiri. Kwani ufalme wa Mungu siyo ufalme wa pupa, uwepo wa Mungu hubadilisha dunia pole pole. Tunapokuwa waaminifu kwa vitu vidogo vidogo katika maisha yetu, tunaendelea kuiotesha mbegu ya ufalme wa Mungu. Baadaye hutaweza kuamini ni kiasi gani umegusa mioyo ya watu kwa jinsi ulivyokuwa mzuri kwao. Ninapo adhimisha miaka sita ya upadri, ninashindwa hata kuamini ninapopata ujumbe ambao watu wanashuhudia jinsi nilivyowagusa. Mara nyingi, hata mimi mwenyewe nsikumbuki kama nilimgusa yeyote kutokana na mahubiri, semina ama ushauri. Mungu anatuambia siku ya leo, tuwe waaminifu, tusikate tamaa kwani ufalme wake haushuhudiwi kwa kufanya mambo makubwa makubwa. Ufalme wa Mungu ni njia ama mtindo wa kuishi na siyo mwisho wa safari. 

Shamba la Ngano:

Read more...